Wanafunzi watoa neno kwa Rais Samia ujenzi shule mpya

Sehemu ya Majengo ya shule mpya ya sekondari Mkabuye iliyopo wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.

WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Mkabuye iliyopo wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wametoa shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo hali iliyosababisha kuondokana na adha mbalimbali ikiwemo kutembea umbali mrefu kwenda shule na kurudi.

Wametoa kauli hiyo kwa timu ya waandishi wa Habari waliotembelea shule hiyo ambapo wamesema kuwa baada ya kuhamishwa kutoka shule ya sekondari ya awali ya Itaba na kuanza masomo kwenye shule hiyo ya Mkabuye mwaka 2023 wanaamini serikali inawajali wananchi wake bila kubagua.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Mkabuye, John Aborgast.

Mwanafunzi wa kidato cha nne John Aborgast amesema adha ilikuwa kubwa maana walilazimika kuamka mapema asubuhi ili kutembea umbali wa zaidi ya kilometa sita kufika shule hivyo hata usomaji wao ulikuwa na changamoto kubwa.

Advertisement

Naye Mwanafunzi Zelekia Herman amesema kwao imekuwa ukombozi mkubwa kwani adha ya kutembelea umbali mrefu na changamoto nyingine hasa kwa wasichana zimepungua.

Mwanafunzi Shule ya Sekondari Mkabuye, Zelekia Herman.

Akizungumzia ujenzi wa shule hiyo Makamu Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari ya Mkabuye, Mwl Damiano Fubusa amesema serikali imetoa sh milioni 603 ambazo zimewezesha kujengwa kwa madarasa 13, jengo la utawala, maabara za sayansi, jengo la Maktaba na jengo la TEHAMA lenye vifaa vyote.

Amesema ujenzi huo umesaidia kupunguza umbali, msongamano na changamoto za baadhi ya wanafunzi kupanga nyumba ili kupata wasaa mzuri wa kupata masomo jambo ambalo kwa sasa halipo tena.

Kaimu Afisa elimu Sekondari wa Halmashauri ya wilaya Kibondo, Respiuce Nkwaitabo.

Aidha kufuatia ujenzi wa shule hiyo Kaimu Afisa elimu Sekondari wa Halmashauri ya wilaya Kibondo, Respiuce Nkwaitabo ameema shule imejengwa kupitia mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari (SEQUIP) na kuifanya Halmashauri hiyo kuwa na shule 24 za sekondari.

Nkwaitabo amesema ujenzi wa shule hiyo umeongeza chachu ya wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kutokana na kuwepo kwa maabara za sayansi na kompyuta lakini pia umesaidia kuondoa utoro ambapo kwa sasa mahudhurio ya wanafunzi ni makubwa.

22 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *