Wananchi Mugoma wafurahia mradi wa barabara

WANANCHI wa Kata Mugoma Wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera wameishukuru serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa kurahisisha mawasiliano ya barabara ya Uzunguni na kuwapunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu kutoka Mgoma kwenda Ngara Mjini.

Mradi wa barabara ya Uzunguni umejengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Oktoba 2023 hadi Juni kwa thamani ya Sh milioni 284 na kupunguza changamoto ya kutembea kwa muda mrefu .

Mchungaji Aneth Mzungu mkazi wa mtaa wa Uzunguni amesema kuwa moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo katika barabara hiyo ni vyombo vya usafiri kushindwa kupanda mlima na kusababisha ajali, pamoja na wananchi wanaoishi mtaa huo kutofikishiwa huduma nyingine kwa urahisi kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

“Haikuwa rahisi kupata bidhaa au serikali kuleta huduma au mtu kufungua biashara, barabara ilijaa tope wananchi walilazimika kufanya mzunguko mkubwa na kutumia gharama kubwa kuja mjini, lakini kwa sasa imerahisishwa na wanachi wanakatiza na huduma nyingi sana zimetufikia huku wengine wakijenga nyumba za kisasa kutokana na uwepo wa barabara nzur,” Mzungu amesema.

SOMA: Mwenge kupitia miradi ya Sh bilioni 30 Mtwara

Edmund Eston mkazi wa Uzunguni anayejihusisha na kutoa huduma za kusafirisha abiria amesema mara kadhaa aligombana abiria kwa kuwapitisha katika barabara hiyo hata hivyo baada ya matengenezo hayo hajapata changamotoo yoyote huku akiipongeza serikali kwa kuwajali wananchi wake.

Mbunge Jimbo la Ngara, Ndaisaba Ruholo amesema uwepo wa barabara hiyo ni faraja kwa wananchi kwani mpaka sasa hajapata malalamiko ya ajali wala changamoto yoyote.

SOMA: Mwenge kukagua miradi 87 Tanga

Kiongozi mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amewapongeza Tarura kwa kuendelea kutekeleza miradi ya viwango na kufuata mfumo wa kidigtal wa manunuzi huku akiwataka wananchi kutumia fursa ya barabara hiyo inayounganisha kata mbili katika kuhakikisha wanakuza uchumi wao.

Meneja Tarura Ngara, Makoro Magoti amesema  fedha za mradi wa barabara hiyo ambayo ilikuwa kero kwa wananchi imetokana na tozo ya mafuta huku akitaja moja ya faida kubwa ya kukamilika kwa mradi huo kuwa ni usafiri na usafirishaji kwa wananchi wanaosafirisha bidhaa kutoka sehemu mbalimba na kuzifikisha kwa wananchi kwa urahisi.

SOMA: Mwenge wa Uhuru wakagua miradi ya Sh Bil 5 Iramba

“Kulikuwa na mmomonyoko mkubwa katika barabara hii, matengenezo yasiyoisha ,uchafuzi wa mazingira ,bidhaa kutoingia kabisa na wananchi kukosa huduma ila mpaka sasa hakuna kikwazo tena na sisi Tarura tunashuhudia wananchi walivyojenga nyumba za kisasa baada ya barababara kukamilika,” amesema Magoti.

Habari Zifananazo

Back to top button