Wananchi Selela waishukuru GEF mradi wa maji

ARUSHA: WANANCHI wa kijiji cha Selela, Kata ya Selela, Wilaya ya Monduli, Mkoa Arusha, wameshukuru Mfuko wa Mazingira Duniani(GEF)  kupitia programu ya ruzuku ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira kwa kufanikisha mradi wa maji kutoka katika chanzo cha maji cha  Kabambe ambacho kimekuwa na manufaa makubwa.

Mradi huo umetekelezwa na Shirika la Waandishi wa habari la Kusaidia Jamii za Asili la  (MAIPAC ) ikiwa ni sehemu ya mradi wa kuheshimu na kulinda maarifa ya jamii za asili katika uhifadhi (Respecting and Preserving Indigenous Traditional Knowledge in Conservation) ambao pia umetekelezwa katika jamii wa Wahdzabe katika eneo la bonde la Eyasi wilaya ya Karatu.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Longidonyi Lunda akiwa pamoja na viongozi wa kamati ya maji na mazingira ya kijiji hicho, amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa uzio kulinda chanzo cha maji cha Kabambe umeongeza maji kwani sasa hakuna tena uvamizi wa watu, mifugo na wanyamapori katika eneo hilo.

Lunda amesema kwa sasa maji yanapatikana ya kutosha katika kijiji hicho kwa ajili ya watu kunywa na kilimo ambacho kinategemea maji ya umwagiliaji na  sasa heka moja inamwagiliwa kwa masaa manne tu tofauti na kabla ya kujengwa uzio wa kutunza chanzo hicho cha maji ambapo heka ilimwagiliwa kwa zaidi ya masaa sita kutokana na uchache wa maji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button