Wanasayansi wabaini mimea ya asili ya ‘kutibu’ pilipili manga

WANASAYANSI wamebaini uwepo wa mimea ya asili inayoweza kudhibiti ugonjwa wa mnyauko na udondoshaji vikonyo vya matunda kwenye zao la pilipili manga.

Wanasayansi hao ni kutoka katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT).

Kudondoka kwa vikonyo kumekuwa tatizo kubwa kwa wakulima wa zao hilo linalotegemewa sana kibiashara na wakulima wa Wilaya ya Morogoro.

Advertisement

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo mtafiti Aloyce Bwire alisema kuwa baadhi ya tafiti zilizofanywa zimebaini ugonjwa huo unasababishwa na uwepo wa fangasi jamii ya fusari na pia rutuba hafifu kwenye udongo.

Aidha, Bwire alisema kuwa utafiti huo umebaini mmea aina ya ‘komfrei’ na mlonge kuwa ndio yenye uwezo mkubwa wa kuzuia ukuaji wa fangasi jamii ya fusari na pia mbolea inayotokana na mimea hiyo ina uwezo wa kuzuia unjano wa majani, manyauko na udondoshaji wa vikonyo vya matunda kwenye pilipili manga.

Utafiti huo ulifanyika katika maabara ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) na kwenye mashamba kwa kushirikisha vikundi vya wakulima wa pilipili manga wa Kijiji cha Kibwaya kilichopo Wilaya ya Morogoro.

Kwa upande wake Ofisa mwezeshaji kutoka SAT, Salma Yasin alisema kuwa pilipili manga ni moja ya viungo vya zamani na vinavyotumiwa sana duniani na hivyo taasisi yake imekuwa ikifanya utafiti kuondoa changamoto wanazokumbana nazo wakulima.

Pilipili manga mkoani Morogoro imekuwa ikilimwa katika kata ya Mkuyuni, Kinole, Kibwaya, Tegetelo na Kibobwa zilizopo Wilaya ya Morogoro.

Pilipili manga kwa sasa huuzwa Sh 7,500 hadi 8,000 kwa kilo moja.