Wanawake ni chachu ya haki, usawa na amani

SIKU ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8, kila mwaka hivyo kesho wanawake wa Tanzania wataungana na wengine duniani kote kuadhimisha siku hii muhimu kwa jamii.

Shughuli na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na maandamano, makongamano, mikutano, semina, warsha na kutembea makundi ya wahitaji zitafanyika kudhihirisha umuhimu na thamani ya mwanamke katika jamii.

Kila mwaka huwa na kauli mbiu na mwaka huu Waziri wa Maendeleo Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu,

Advertisement

Dk Dorothy Gwajima hivi karibuni akitangaza maadhimisho rasmi ya siku hiyo alisema kauli mbiu mwaka huu ni, ‘Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji’.

Kauli mbiu hii inaakisi ya Kimataifa isemayo, ‘Kwa Wanawake na Wasichana Wote, Usawa, Haki na Uwezeshaji’.

Ni dhahiri kauli mbiu hii imelenga kuhamasisha jamii kukuza usawa, haki na uwezeshaji wa wanawake na wasichana hasa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Tunashauri wanawake wanapoadhimisha siku yao kesho na kwa kuzingatia maana halisi ya kauli mbiu ya mwaka huu, wakumbuke wanapaswa kujiamini, kujiandaa na kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.

Lakini pia wanawake watumie maadhimisho haya kutathmini mafanikio yao, kuinuana kuanzia ngazi za mitaa na kuhamasishana kushiriki katika maendeleo kwa usawa wa kijinsia.

Ni matumaini yetu maadhimisho haya yatatumika pia, kama fursa ya kuelimishana na kukumbushana kuwa mwanamke si nafasi ya kupendelewa kuliko jinsi nyingine ila ni udhihirisho wakipewa fursa na nafasi wana nguvu na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi na weledi mkubwa.

Mfano halisi wa hili ni Rais aliye madarakani, Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na viongozi wengine wengi.

Wakati umefika sasa pia, jamii iondokane na dhana iliyojengeka kuwa usawa wa kijinsia unabagua wanaume ilhali kila upande unamtegemea mwenzake kwa maana hawezi kuwepo mwanamke bila kuwepo mwanaume na hawezi kuwepo mwanaume bila mwanamke.

Jamii inapaswa pia, kutambua Siku ya Wanawake Duniani haiko kuonesha mgawanyo wa kijinsi, nguvu ya mwanamke dhidi ya mwanaume; la hasha, bali kuonesha ulimwengu ni namna gani wanawake wamepiga hatua ya kimaendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa na mchango wao kwa ustawi wa nchi kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Tunawaunga mkono wanawake kupitia kauli mbiu ya mwaka huu kuhakikisha jamii inaimarisha haki, usawa na uwezeshaji na kufanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi. Kila la heri kwa wanawake na wasichana, 2025 uwe mwaka wa mafanikio makubwa zaidi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *