Watoto milioni moja kupatiwa chanjo ya polio Geita

JUMLA ya watoto 1,114,918 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya polio mkoani Geita kupitia awamu ya kwanza ya utekelezaji wa kampeni ya chanjo hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Omary Sukari ametoa taarifa hiyo hiyo katika hafla ya kutambulisha kampeni hiyo na kueleza awamu hiyo ya kwanza ya chanjo itaanza Machi 24 hadi Machi 27, 2026.
Amesema mkoa umepokea dozi za chanjo ya polio zipatazo milioni 1.3 ambapo maandalizi ya chanjo yamekamilika na watumishi wa afya zaidi ya 6000 wamejengewa uwezo tayari kufanikisha chanjo hizo.
“Dunia kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kuondosha ugonjwa wa polio, lakini bado zipo nchi ambazo zina visa vya ugonjwa wa polio na ndani ya nchi yetu kwa muda mrefu tulikuwa hatuna hivi visa.
“Ili kutokomeza kabisa njia pekee ni kuhakikisha watoto wetu wanapata chanjo,wanakingwa dhidi ya ugonjwa wa polio,” amesema Dk Sukari
Ofisa Mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Michael Ndowa amesema kuwa kampeni ya chanjo ya matone ya polio inatarajiwa kutolewa katika mikoa saba.
Ameitaja mikoa hiyo ni Mwanza, Mara,Tabora, Shinyanga, Simiyu, Singida na Geita akieleza kuwa inatarajiwa kutolewa kwa zaidi ya watoto milioni sita katika mikoa hiyo walio na umri chini ya miaka 10.
Amesema hatua ya utolewaji wa chanjo hiyo imekuja kufuatia matokeo ya ufuatiliaji yaliyofanywa na Wizara ya Afya kubaini uwepo wa kiashiria cha kirusi cha polio katika moja ya sampuli iliyopimwa mkoani Mwanza.



