Watu 30 kupandikizwa nyonga, magoti
JUMLA ya watu 30 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa upandikizaji wa nyonga na magoti katika kambi ya siku tano iliyoanza leo kwa watu sita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohammed Janabi amesema tangu kuanza kwa huduma hiyo mwaka 2022 tayari watu 173 wamepata huduma hiyo.
“Hadi sasa tuna wataalamu sita ambao wanauwezo wa kufanya upandikizaji huo na serikali ninajenga uwezo kwenye sehemu zaidi ya moja kwani hata MOI wanatoa huduma na sisi tunatoa hii inasaidia sana wananchi kupata matibabu kwa urahisi.
SOMA: Muhimbili kuanza kuhifadhi mbegu za uzazi
Prof Janabi amesema gharama za upandikizaji huo ni Sh milioni saba hadi Sh milioni 10 huku wale wenye Bima za Afya gharama zao asilimia 90 zinalipiwa.
Amebainisha kuwa upasuaji huo utaendelea kufanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi ambapo sasa wapo madaktri kutoka India na pia hospitali hiyo itafundisha wataalamu wa hospitali zingine.
“Upasuaji ukifanyika hapa ndani gharama zinapungua kuliko kusafiri kwenda nje na sasa uhitaji ni mkubwa hata vijana wa miaka 30 na 40 wanapata matatizo haya kutokana na mtindo wa maisha.
SOMA: Muhimbili yavuna mbavu, yatengeneza taya
“Kuna suala la ukomo wa hedhi hili kwa wanawake linasumbua kwani wanapata matatizo ya nyonga na magoti lakini kikubwa mtindo unachangia,”amesisitiza.
Mmoja wa wagonjwa walionufaika na matibabu hayo, Sunday Manara ametoa shukrani kwa hospitali kwa kutoa huduma nzuri na kutaka watanzania wajivunie vya kwao.
“Huduma hii najivunia nina miaka 82 sasa ninamatumaini baada ya kufanyiwa upasuaji na najitahidi kufuata masharti niliyopewa na madaktari na natoa wito kwa wananchi tumekuwa nyuma kusifia vitu vyetu kitu ambacho sio sahihi Mloganzila ni sehemu nzuri kwa matibabu,”ameeleza.