Watuhumiwa kuiba vifaa vya ujenzi vya serikali

Makandarasi ‘goigoi’ waikera serikali

WATUMISHI wanane wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita wanashikiliwa kwa tuhuma za kuiba vifaa vya ujenzi .

Vifaa hivyo vilikuwa vimehifadhiwa tayari kwa matumizi ya miradi ya ujenzi ikiwemo nyumba za watumishi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamhuri William amethibitisha hilo juzi katika kikao cha nne cha baraza la madiwani kilicholenga kujadili utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2021/2022.

Advertisement

Alitaja watuhumiwa hao kuwa ni Ofisa Afya wa Idara ya Uzazi wa Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Nyang’hwale, dereva wa halmashauri na mlinzi mmoja huku watumishi wengine watano wa idara tofauti taarifa zao hazijawekwa wazi.

Alibainisha kuwa watumishi hao wanatuhumiwa kuiba mabati 60 ya geji 28 na makasha 20 ya vigae ambavyo vilipotea katika mazingira ya kutatanisha.

“Ni vyema wakuu wa idara wakachukua hatua ili kurekebisha kasoro kama hizo, kwa mtumishi kukutwa ameiba mabati, ameiba vigae kwanza ni aibu kwa sababu serikali inawalipa mishahara, inawalipa posho na marupurupu”.

“Sisi kama Kamati ya Ulinzi na Usalama tunalifuatilia jambo hili kwa ukaribu, kwa umakini, ili wote waliohusika wachukuliwe hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria, na hili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo ili masuala kama haya yasijirudie tena,” alieleza.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, John Izack alivipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kudhibiti wizi huo na kuagiza uchunguzi ufanyike ili wote waliohusika hatua za kisheria zichukuliwe.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale, Rajabu Mmunda aliahidi kushirikiana na wakuu wa idara kufuatilia kwa ukaribu hujuma na vikwazo kwenye baadhi ya miradi ya ujenzi inayotekelezwa.