UONGOZI wa klabu ya Yanga umeweka wazi kwa kusema kwamba una ushindani mkubwa na maadui wakubwa kinachowanusuru ni umoja, mshikamano na mapambano ya dhati kutoka kwa wanachama wa klabu huyo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema mashabiki na wanachama wanapaswa kuwa pamoja na viongozi wao katika mapambano ya kutafuta alama tatu katika kila michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara ili kutetea taji hilo.

“Ligi ni ngumu sio kwamba msimu umemalizika, yanavyozungumzwa huko nje ni tofauti na uhalisia ulivyo, tofauti ni alama moja kwenye msimamo na bado zaidi ya mechi 10.

Kimsingi bado pointi 30 zipo nje kupigania, tuna nafasi ya kuuchukua ubingwa wetu kwa sababu mwisho wa siku tujivunie kile tulichokipata mwisho na sio kupiga hesabu hapa katikati, ligi bado sana, hivyo wanayanga tusimame na tuzibe masikio yetu,” amesema.

Kamwe amesema wanayanga wasikaribishe maneno yanayozungumzwa na wapinzani wao kwa sababu muda wa kutafuta alama tatu kila mechi wanao na mwisho wa msimu majibu ya ubingwa yatakuwa hadharani.
Yanga inacheza mchezo wa Ligi KUU dhidi ya KMC jioni hii kwenye uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.