Yanga kama hawapo vile!

DAR ES SALAAM – YANGA ni kama wanalitafuta jambo lao mdogo mdogo wakizipanga karata zao kukusanya alama kwenye kila mchezo.

Hii ni baada ya jana Mabingwa hao Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuendeleza wimbi la ushindi katika ligi kwa kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC FC, mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi Dar-es-Salaam. Bao pekee la Yanga kwenye mchezo huo lilifungwa na Max Nzengeli dakika ya 5 ya mchezo.

Ushindi huo ni watatu kwa timu hiyo msimu huu baada ya kushinda michezo miwili iliyopita na sasa wamefikisha pointi tisa wakiwa wamefunga mabao manne na hawajaruhusu bao mpaka sasa wakiungana na Simba ambao nao hawajaruhusu nyavu zao kuguswa.

Baada ya mchezo huo kocha wa Yanga Miguel Gamondi amesema kwasasa anaangalia zaidi pointi tatu na sio idadi ya magoli wanayoshinda licha ya kukiri ubutu kwenye safu yake ya ushambuliaji. Gamondi amesema licha ya kufurahishwa na ushindi huo bado anaumizwa kichwa na safu yake ya ushambuliaji akitamani matumizi sahihi ya nafasi wanazotengeneza.

SOMA: Ateba – Nitafunga sana tu!

Ikumbukwe Yanga kwa sasa ina washumbuliaji wanne Prince Dube, Kennedy Musonda, Jean Baleke na Clement Mzize lakini mpaka kufikia sasa ni Clement Mzize aliyefunga walau bao moja kwenye Ligi Kuu jambo linalomuumiza kichwa kocha huyo raia wa Argentina.

Katika mchezo huo beki wa kushoto wa Yanga, Chadrack Boka amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ikiwa ni mara ya pili mfululizo kushinda tuzo hiyo.

Michezo mingine ya Ligi Kuu iliyopigwa jana Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Singida Black Stars ikalazimishwa sare ya bao 1-1na maafande wa JKT Tanzania huku Mashujaa wakiibana mbavu Azam Fc kwa kutoka suluhu Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.

Habari Zifananazo

Back to top button