Yanga yaipania Vital O mchezo wa marudiano CAF
YANGA imesema mchezo wa marudiano Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vital O ya Burundi utatumika kuzindua rasmi msimu mpya wa michuano hiyo ya kimataifa huku wakitamba kuwa wamejipanga kushinda idadi kubwa ya mabao.
Mchezo huo wa hatua za awali, utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam Jumamosi ya wiki hii. Ule wa kwanza wa ugenini uliochezwa katika Uwanja wa Azam Complex Yanga ilishinda mabao 4-0.
Akizungumza leo na waandishi wa habari Dar es Salaam, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yanaendelea vizuri na kudai kila mchezaji ana morali ya juu kuhakikisha anapata matokeo na kusonga mbele.
SOMA: Yanga yapewa Vital’O, Azam kuivaa APR
“Wachezaji wote wanaendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha miili yao ili waweze kupata magoli mengi zaidi ya yale tuliyoyapata kwenye mchezo wetu wa awali, tunataka kuondoka na fedha nyingi za Rais Samia Suluhu Hassan za goli la mama,”alisema
Kamwe alisema CAF imeiruhusu kufanya uzinduzi rasmi wa michuano hiyo kutokana na juhudi wanazozionyesha nje na ndani ya uwanja na kuwahimiza mashabiki kujitokeza kwa wingi kujaza Uwanja huo.
“Tumewasiliana na Shirikisho lampira wa miguu Barani Afrika (CAF) wameturuhusu tufanye uzinduzi wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika katika uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ndio tumeuchagua kuwa uwanja wetu wa nyumbani kutokana na mvuto tuliokuwa nao pamoja na kuvutiwa na yale tuliyoyafanya kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi, alisema Kamwe.
View this post on Instagram
Alitangaza viingilio vya kuuona mchezo huo kuwa VIP A ni 30,000 VIP B 20,000 VIP C 10,000 pamoja na viti vya mzunguko 5000.
Meneja huyo aliwataka mashabiki pamoja na wanachama wao kununua tiketi mapema kabla ya kufika siku ya mchezo ili waepuke usumbufu wa kuingia uwanjani hapo,kwani tayari zimeanza kuuzwa.