Zahanati ya Kilulu yafikishiwa jengo mama na mtoto

TANGA: WANANCHI wa kijiji cha Kilulu Duga kilichopo Kata ya Sigaya Wilaya ya Mkinga wameepushwa na kutembea umbali wa kilometa 8 kufuata huduma ya kujifungulia baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka Jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kilulu Duga.
Mradi huo wenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa akina mama na watoto wachanga ni sehemu ya mkakati wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga kwa wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani unagharimu Sh milioni 64.
Akizungumza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula amesema kuwa mradi huo utawasaidia kinamama wajawazito kuweza kujifungua katika eneo salama na bora zaidi ya awali.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa uwekezaji huu ambao Sasa unakwenda kuhakikisha usalama wa mama na mtoto na hivyo kupunguza au kuondoa kabisa vifo vitokanavyo na uzazi,” amesema Naibu Waziri huyo.
Hata hivyo kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi amesema kuwa mradi huo unakwenda kuwa faraja kwa wananchi kutokana na zahanati ya awali kutokuwa na utoshelevu wa kuhudumia watu wengi kutokana na ongezeko la watu katika eneo hilo.
SOMA ZAIDI
Kiongozi mbio za mwenge ataka zahanati kukamilika kwa wakati
“Zahanati hii imezingatia mahitaji ya wananchi, hapa tunayo zahanati ambayo haitoshelezi kwa sababu kuna uhitaji mkubwa wa huduma ya kujifungulia kwa kina mama ambapo serikali hii ya Dk Samia Suluhu Hassan imekuwa sikivu kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri kujenga zahanati nyingine ili kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Ussi.