Samia aagiza ijengwe SGR kwenda Arusha

ARUSHA; RAIS Samia Suluhu Hassani ameagiza uanze mchakato wa kujenga Reli ya Kisasa (SGR) kwenda mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa alisema hayo alipozungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda jijini Arusha juzi.
“Tuna mpango mkubwa sana kwa Arusha kwa maana maelekezo mahsusi ya Rais kuanza ujenzi wa SGR kuja hapa Arusha na itaambaa ambaa kwenda hadi Musoma,’’ alisema Kadogosa.
Alisema ujenzi wa reli hiyo ilikuwa ni matamanio ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
“Walisukuma hadi mahali walipofikia lakini ni matamanio ya Baba wa Taifa kuona kwamba tunaunganisha kutoka Tanga, Kaskazini itumie Bandari ya Tanga ifike Musoma ivuke kwenda Jinja,” alisema Kadogosa.
Alisema ujenzi wa SGR utasaidia kukuza shughuli za kiuchumi ikiwamo biashara ya magadi na nikeli.
“Kuna magadi ambao ni uchumi mkubwa sana yale machimbo yanaweza kuendelea zaidi ya miaka 100, maeneo ya Dutwa kuna nikeli, kwa hiyo kuna sababu za kiuchumi kwanini hii reli ijengwe,” alisema Kadogosa.
Alisema pia reli hiyo itasaidia katika usambazaji wa mafuta kutoka Uganda hadi Tanga.
“Tutakapounganisha na Uganda maana yake utaunganusha na Sudan Kusini ndio maana kwa wenzetu wa bandari wanataka kujenga bandari kavu kubwa pale karibu na KIA (Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro,” alisema Kadogosa.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alisema mradi huo utakapoanza utakuwa ni fursa ya kipato kwa wakazi wa mkoa huo.
“Hata kusambaza kokoto sisi ni hela, malori ya kusambaza mizigo ni hela, hii ni fursa kubwa sana,” alisema Makonda.



