Wananchi Ngorongoro wamshukuru Dk Samia urejeshaji mipaka

ARUSHA: WANANCHI na viongozi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali katika Tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha wamempongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kurejesha maeneo ya vijiji na mipaka iliyokuwa imefutwa awali katika eneo hilo.
Hatua hiyo wameiita suluhisho la matumaini kwa wakazi wa eneo walio ndani ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA).
Wamesema, uamuzi huo umefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya wananchi na NCAA huku miradi ya maendeleo ikiendelea kutekelezwa kwa kasi katika sekta za elimu, maji na afya.
Akizungumza katika vikao vya ndani vya mikakati ya kampeni iliyoshirikisha viongozi na wananchi na viongozi wa milla katika Tarafa ya Ngorongoro yenye kata 11 akiomba kura kuchaguliwa kuwa Mbunge na kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge mteule wa Jimbo la Ngorongoro, Yanick Ndoinyo alisema Rais Samia ameonyesha uongozi wa kipekee unaojali maisha ya wananchi wa Ngorongoro.
Ndoinyo alisema Rais Samia ameleta usawa kati ya uhifadhi na ustawi wa jamii, jambo ambalo halijawahi kufanyika kwa muda mrefu kwani viongozi wengi wa Kitaifa walikuwa wazito kutoa maamuzi hayo lakini mtawala huyo wa sasa ameamua kutekeleza hivyo anastahili kupongezwa kwa dhati.
Mgombea huyo alisisitiza na kusema kuwa wananchi wa eneo hilo hawatakubali kuvurugwa na watu wachache wanaotaka kuhujumu jitihada za maendeleo na kuipatia CCM ushindi wa kishindo utapatikana kwa yeye,mgombea urais na madiwani wote wa chama hicho.
“Tumejipanga kuhakikisha Rais Samia, wabunge na madiwani wa CCM wanapata kura za kutosha. Wananchi wanaona matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa, hasa kwenye miradi inayogusa maisha yao moja kwa moja,” alisema Ndoinyo.
Kwa upande wake, Jemsi Saringe, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Olbalba, alisema kuwa wameweka mikakati kabambe kuhakikisha kila mwananchi anashiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu ujao, huku mabalozi wa nyumba kumi wakipewa majukumu ya kuhakikisha wanapita nyumba kwa nyumba kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na kuichagua CCM katika ngazi zote zinazowania uongozi katika uchaguzi mkuu.
“Tumejipanga vizuri kwani kila kaya itashiriki kupiga kura na kila mwananchi atapiga kura na tunataka ushindi wa kishindo kwa Rais, Mbunge na Madiwani wa CCM,” alisema
Naye Metui Ole Shaudo, Diwani Mteule wa Kata ya Olbalba, alisema kutokana na jiografia ya eneo hilo lililopo ndani ya hifadhi ya kipekee duniani, viongozi wameweka mikakati maalum kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kikamilifu kwenye zoezi la kupiga kura siku ya octoba 29 mwaka huu.
“Tumeamua mifugo ipelekwe malishoni siku moja kabla ya uchaguzi, na pia tumeandaa usafiri kwa wazee na wanawake ili kila mmoja aweze kushiriki bila kikwazo,” alisema Shaudo
Diwani huyo mteule alisema kuwa viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wameahidi kulipa fadhila kwa Rais Samia kupitia kura na wamesisitiza kuwa ahadi zake za maendeleo hazijabaki maneno bali zinajidhihirisha kwa vitendo.