Biteko ateta na Jumuiya ya Wasambazaji mitungi ya gesi nchini

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Kampuni zinazohusika na Usambazaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) -TZLPGA kwa lengo la kuwashukuru kwa mchango wao katika utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo utatuzi wa changamoto zinazoikumba TZLPGA ili kuhakikisha wanatoa huduma kwa urahisi nchi nzima.
Mazungumzo kati ya Dk Biteko na Jumuiya hiyo yamefanyika leo Februari 20 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja watendaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA).

“ Ili Serikali ifanikiwe lazima kuwashirikisha watu wake, tunawashukuru sana kwa mchango wenu katika kufanikisha Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ambao kutoka tuuzindue mwaka 2024, uelewa na matumizi ya mitungi ya gesi umeendelea kuongezeka, mitungi hii ni gharama lakini ninyi mnajitoa na kutuunga mkono,” amesema Dk Biteko.
Hata hivyo Dk Biteko amezitaka kampuni hizo kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa mitungi ya gesi inafika kwa wingi hadi ngazi ya vijiji ili kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 75 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030 ikiwa pia ni utekelezaji wa Mpango wa Mahsusi wa Nishati ( Energy Compact) uliosainiwa mwezi Januari 2025.

Amesema lengo la kikao hicho pia lilikuwa ni kujadili changamoto ambazo kampuni hizo wanakutana nazo zikiwemo za kikodi ambazo zina nafasi ya kujadiliwa katika Muswada wa Masuala ya Fedha utakaosomwa katika Bunge la Bajeti la mwaka 2025/2026.
“Tumekutana hapa ili tunapoelekea kwenye Bajeti ya Serikali mtuambie kipi tukiboreshe kupitia Muswada wa Masuala Fedha na ni vizuri pia mkatueleza jambo gani lifanyike ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” ameeleza Dk Biteko.