BoT yapunguza riba ya mikopo

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imepunguza riba yake kutoka asilimia sita hadi 5.75.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema hayo wakati akitangaza uamuzi wa kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha.
Amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.
Tutuba alisema Dar es Salaam kuwa riba hiyo inaanza kutumika mwezi huu hadi Septemba mwaka huu.
Alisema kiwango hicho kimeshuka ikilinganishwa na riba ya asilimia sita iliyokuwa ikitozwa kwa vipindi zaidi ya viwili vilivyopita.
Alisema BoT ilianza utaratibu wa kutangaza riba yake kila mwanzo wa robo ya mwaka tangu walipoanza kutekeleza mfumo mpya wa sera ya fedha unaotumia riba Januari 2024.
Alisema Kamati ya Sera ya Fedha imebaini uchumi umeendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha ukichochewa na uwekezaji wa serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.
Kuhusu uchumi wa ndani alisema uliendelea kuwa stahimilivu na unatarajiwa kuendelea kuimarika.
Alisema uchumi wa Tanzania Bara ulikadiriwa kufika asilimia 5.8 katika robo ya kwanza na asilimia 5.5 katika robo ya pili ya mwaka 2025.
Ukuaji huo umechangiwa zaidi na sekta za kilimo, ujenzi na huduma za fedha na bima.
Alisema uchumi wa ndani unatarajiwa kuendelea kuimarika na unatarajiwa kufikia asilimia 6.0 na 6.9 katika robo ya tatu na ya nne, mtawalia.
Alisema imani ya wawekezaji imeendelea kuimarika kama inavyoonekana kwenye matokeo ya tathmini iliyofanywa na Kampuni ya Fitch, Juni mwaka huu iliyothibitisha daraja la B+ kwa Tanzania.
Alisema mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara ulikuwa wastani wa asilimia 3.2 katika robo ya pili ya mwaka 2025.
Upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei ulipungua hadi asilimia 4.2 Mei mwaka huu kutoka asilimia 5.3 mwaka mmoja uliopita hali iliyochangiwa zaidi na kushuka kwa bei za chakula.
Alisema Shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa tulivu dhidi ya sarafu nyingi za kigeni.
Utulivu huo umechangiwa zaidi na kuongezeka kwa ukwasi wa fedha za kigeni kutokana na mapato ya utalii na mauzo ya bidhaa nje ya nchi, hususani dhahabu na tumbaku.
Pia, alisema utekelezaji wa sera ya fedha na usimamizi wa kanuni zinazotaka miamala ya fedha ya ndani ya nchi kufanyika kwa Shilingi vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha utulivu wa Shillingi.
Aidha alisema ongezeko la ununuzi wa dhahabu kutoka ndani ya nchi kwa ajili ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni lilichangia kuongeza imani kwa sarafu ya Tanzania.
Tutuba alisema tangu BoT ianze kununua dhahabu iliyosafishwa Oktoba Mosi, mwaka jana hadi Juni 30, mwaka huu wamenunua tani 6.6 za dhahabu hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 718.
“Lengo letu lilikuwa kila mwaka tununue dhahabu safi tani sita, mwaka huu tumevuka lengo tumenunua tani 6.6 na mwaka huu mpya ulioanza tutaendelea kununua dhahabu kama tulivyojiwekea lengo,” alisema.