CCM yaja kivingine, mikutano sasa kidijiti

DODOMA; CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kinazindua ilani yake 2025-2030 kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema ilani hiyo imezingatia weledi na imeshirikisha wananchi, asasi za kiraia, taasisi za elimu ya juu na wadau wengine wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Rais Samia alisema hayo Dodoma jana wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM unaomalizika leo.
Alisema Ilani ya 2020-2025 iliakisi kipindi cha kwanza na ilani inayozinduliwa leo inaakisi kipindi cha pili na cha mwisho cha utekelezaji, mwelekeo wa sera za CCM katika mwaka 2020-2030.
Rais Samia alisema anatarajia baada ya uzinduzi wa ilani leo wajumbe kwa pamoja wataifikisha na kuitangaza kwa wananchi wakati utakapofika.
“Itakuwa sambamba na kutangaza kwa wananchi mafanikio ya ilani ya CCM katika utekelezaji wa ilani iliyopita,” alisema.
CCM imefanya mabadiliko madogo matatu katika Katiba yake ya Mwaka 1977 Toleo la Januari 2025 na sasa vikao vya chama kwa ngazi ya wilaya hadi taifa vitafanyika kwa njia ya mtandao endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo au dharura.
Pia, kimefanya marekebisho ya kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa miradi ya chama kwa Baraza la Wadhamini la CCM kutoa idhini ya maandishi kwa Kamati ya Siasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa na taasisi za chama.
Rais Samia alisema mabadiliko hayo yanafanywa kuboresha utendaji wa kazi za chama.
“Kama mnavyojua Chama Cha Mapinduzi kinaenda jinsi dunia inavyoenda, CCM sasa inafanya kazi kidijiti na tumefunga mitambo ya mawasiliano na mkoa na wilaya ili kurahisisha utendaji kazi,” alisema.
Aliongeza: “Kwa sasa tumekuja na wazo la e-meeting (mkutano mtandao) ambayo idara ya oganaizesheni inapendekeza vikao vya kufanyika kwa njia ya mtandao.”
Rais Samia alitaja vikao hivyo ambavyo vitafanyika kwa mtandano endapo kuna ulazima wa kufanya hivyo ni vikao vya sekretarieti za wilaya na kamati ya siasa ya wilaya na sekretarieti ya mikoa na kamati ya siasa ya mikoa.
Vingine ni Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Halmashauri Kuu CCM Taifa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa.
“Baada ya mabadiliko tutakwenda kuandaa kanuni za kusimamia vikao hivi ambavyo tumetaka Katiba ivitambue ili kusiwe na shida,” alisema Rais Samia.
Aliongeza: “Vikao husika kwa mkoa na wilaya vitafanyika kwa njia ya mtandao endapo tu kuna ulazima au kuna dharura, lakini pia vitafanyika kwa idhini ya Katibu Mkuu baada ya kueleza sababu, lengo ni kuepusha kutumika vibaya.”
Rais Samia pia alisema mabadiliko mengine ni kuongeza idadi ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini kutoka wajumbe wanane wa sasa hadi tisa ili kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa inayotaka idadi ya wajumbe wa baraza hilo katika vyama vya siasa kuwa ni ile isiyogawanyika kwa mbili.
Pia, alisema marekebisho ya katiba hiyo ni kwa Baraza la Wadhamini kutoa ridhaa ya maandishi kwa kamati za siasa za mikoa na taasisi za chama katika kubuni na kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Kwa mtazamo huo ni wakati muhimu kwa Baraza la Wadhamini la CCM kuona, kujiridhisha na kutoa maelekezo ya miradi itakayobuniwa na ngazi za mikoa na taasisi nyingine za chama kwa manufaa ya chama,” alisema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia alisema kutokana na utekelezaji wa mradi wa kusajili wanachama kwa njia ya kielektroniki mpaka jana CCM ilikuwa na wanachama 13,000,670.
Imeandikwa na Anastazia Anyimike (Dodoma) na Zena Chande (Dar).