COSTECH yawapa kipaumbele watafiti wanawake

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH), Dk. Amos Nungu amesema Tume hiyo imewapa watafiti wa kike na watafiti wachanga nafasi ya kiupaumbele kwani kundi hili linahitaji msukumo ili kuonesha uwezo wake.

Amesema hayo leo Dar es Salaam mara baada ya Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya utekelezaji wa programu ya Kizazi chenye Usawa (GEF) kufanya ziara COSTECH.

“Mwaka jana tulifadhili utafiti wa kuangalia usalama wa chakula na tulikuwa na tafiti nne ambapo viongozi wa tafiti hizo walikua wanawake hii ilikua nafasi ya wao kuweza kubuni na mfano mzuri,” amesema Dkt Nungu.

Advertisement

Kwa upande wake kamati hiyo imevutiwa na juhudi zinazowekwa na taasisi pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa za kukua katika teknolojia na sayansi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo mmoja wa wanakamati, Grace Munisi amesema wanakamati wamefurahishwa na mikakati na mipango ya Tume ya Sayansi na Teknolojia katika ushirikishaji wanawake na Vijana katika teknolojia ya ubunifu na sayansi kwa ujumla kupitia tafiti mbalimbali nchini.

Soma: Vituo vya malezi na makuzi fursa kwa wanawake

“Tume hii ya sayansi ya teknolojia ina juhudi za makusudi za kumuinua mwanamke na kijana kiteknolojia na hii inaenda sambamba na agenda ya Rais katika kumuwezesha mwanamke kiuchumi na hii italeta matokeo makubwa kwa nchi, “amesema Grace.

Aidha wakati Kamati hiyo ikiwa katika Kituo cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Kigamboni Mwalimu wa kituo hicho Martha Njogolo amesema kituo kimeweza kuwapunguzia wanawake mzigo wa ulezi kwani uwepo wa kituo hicho kunawasukuma kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

“Kwa mazingira ya sasa ni vyema zaidi mtoto kushinda katika kituo cha elimu ya awali kwani anakua salama zaidi lakini pia anapata nafasi ya kucheza na wenzake pamoja na kujifunza vitu ambavyo vitaimarisha ukuaji wa ubongo wake,” amesema Martha.

Ikiwa katika ziara Zanzibar Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa Programu ya Kizazi Chenye Usawa ilizitaka taasisi zinazohusika na uwezeshaji wananchi kiuchumi kuweka mkakati wa kuungana kufanya kazi kwa pamoja ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokwaza ufikiaji wa haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake.