Hujuma yakosesha umeme wilaya tatu Kigoma
WATU wasiojulikana wamehujumu miundombinu ya Gridi ya Taifa ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoka kituo cha Nyakanazi Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera kupeleka nishati hiyo mkoani Kigoma.
Hujuma hiyo ilisababisha wilaya tatu za Mkoa wa Kigoma zikose umeme.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kigoma, Jafari Mpina alisema mjini Kigoma jana kuwa tukio hilo limetokea kwenye Kijiji cha Itumbiko wilayani Kakonko katika Mkoa wa Kigoma usiku wa kuamkia jana.
Mpina aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika hujuma hiyo watu hao walichoma moja ya nguzo zinazosafirisha umeme huo, wakang’oa vyuma kwenye baadhi ya nguzo hizo na kisha kuandika mabango kwamba umeme usipopelekwa eneo la Kijiji cha Itumbuko hujuma hizo hazitaisha.
Alisema walizima umeme huo tangu alfajiri ya jana na matengenezo kwa ajili ya kuweka miundombinu mingine ilikuwa imeanza.
Wilaya zilizoathirika na hujuma hiyo ni Kakonko, Kibondo na Buhigwe ambazo ziliungwa kwenye gridi ya Taifa wiki iliyopita.