Miguu kifundo ni tatizo linalotibika likiwahiwa

MIGUU kifundo au nyayo zilizopinda ni aina ya ulemavu unaotokana na matatizo ya mifupa ambayo humtokea mtoto yeyote baada ya kuzaliwa. Wataalamu wanaeleza kuwa hakuna sababu sahihi inayohusishwa na watoto kuzaliwa na miguu yenye kifundo lakini pia kuna uwezekano mkubwa wa mtoto kuzaliwa kama wazazi au mzazi mmoja alikuwa na ulemavu huo.

Aidha, wataalamu hao wanasema katika kila vizazi hai 1,000 kuna uwezekano kuzaliwa kwa mtoto mmoja au wawili wenye nyayo zilizopinda. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya zinaonyesha kuwa watoto 2,000 hadi 2,800 wanazaliwa na mguu kifundo kila mwaka nchini Tanzania.

Daktari wa Mifupa kutoka Hospitali ya CCBRT Zainabu Ilonga akinukuliwa kupitia mitandao ya kijamii anasema wakunga, wauguzi na wazazi wanapaswa kuwa wa kwanza kugundua tatizo hilo kabla ya watu wengine. Ilonga anasema kawaida mtoto mwenye tatizo miguu huangalia chini au ndani, wakati mwingine mguu unakuwa mfupi au imetazamana chini na inaangaliana kwa kuangalia ni rahisi kumgundua.

Ilonga anasema lazima tuanze matibabu akiwa na wiki mbili tangu kuzaliwa anapozidi kucheleweshwa kupata matibabu mifupa na misuli inakomaa. “Sisi tunaanza kufunga POP ili kunyoosha mifupa, akija umri mkubwa anaweza kuhitaji upasuaji mkubwa lakini akifika mapema anafungwa POP na baadaye kuvalishwa viatu,” anasema Ilonga.

Mtaalamu wa mazoezi tiba kwa watoto wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Prisla Mselle anasema madhara yatokanayo na nyayo zilizopinda ni maumivu makali wakati wa kutembea na kushindwa kutembea vizuri na kushindwa kuvaa viatu kama watoto wengine.

Akizungumza na HabariLEO Mselle anasema watoto wenye nyayo za aina hii hukumbana na unyanyapaa na kutengwa na wenzao katika jamii na wakati mwingine wasipopatiwa matibabu na kukua na ulemavu huo humfanya kuwa na hali ngumu kiuchumi. Mselle anasema zaidi ya watoto watano wenye ulemavu wa mguu kifundo hufikishwa katika hospitali hiyo kwa mwaka na wazazi hulazimika kuhudhuria kliniki kwa ajili ya matibabu ya watoto wao.

“Hatua za kwanza za matibabu huchukuliwa kwa mtoto anayezaliwa akiwa na hali ya mguu kifundo kwa kufungwa hogo (P.O.P) kuanzia mapajani hadi katikati ya vidole vya miguu,” anasema Mselle. Mselle anasema mtoto anapofungwa hogo mzazi au mlezi yampasa kuwa makini ili isiingie maji, mkojo wala kinyesi pia kutoning’iniza miguu ya mtoto pale anapo mbeba na kumuweka juu ya kitanda anachomlaza.

“Kuna hali za hatari mzazi au mlezi anatakiwa kuzizingatia ambazo ni vidole kubadilika rangi kuwa rangi ya bluu au nyeusi, vidole kuvimba au hogo kushuka na kusababisha vidole kuzama ndani ya hogo alilofungwa,” anasema Mselle. SOMA: Madaktari wasisitiza miguu vifundo, matege yanatibika

Mselle anasema mtoto anafanyiwa upasuaji mdogo na baadaye tena kuendelea na ufungwaji wa hogo kwa muda wa wiki tatu, hatua ya mwisho atavaa viatu maalumu baada ya kushauriwa na mtaalamu wa afya kutoka hospitalini. Mzee wa kimila kutoka wilaya ya Shinyanga Sonda Kabeshi anaeleza kuwa zamani kabla ya kugundua matatizo ya miguu kifundo kuwa yanatibika baadhi ya wazazi walikuwa wanafikiri ni masuala ya ushirikina.

Kabeshi anasema wazazi hasa wakiume walikuwa wakikimbia familia wakiona hali ya mtoto kuwa hivyo na kuona ni laana ndani ya familia au ukoo wakati mwingine ilimfanya mzazi au mama kutengwa na mwanaye. “Kadri siku zinavyoenda na kuingia kwa utandawazi jamii imeelimika angalau wanapata vitu vingi ikiwemo viongozi wa dini kuhubiri na baadhi ya mila kandamizi kupuuzwa,” anasema Kabeshi.

Mkazi wa Kata ya Mwawaza, Manispaa ya Shinyanga, Mwajabu Kanyenye ambaye alijifungua mtoto mwenye miguu kifundo anasema alimgundua mwanaye wa umri wa mwaka mmoja sasa kwamba ana tatizo hilo pale alipofikisha umri wa kutaka kusimama.

“Nilimpeleka kliniki nikawaeleza lakini wakanishauri niende hospitali ya Rufaa ya Mkoa nikakutana na wataalamu wakamfunga mtoto wangu POP lakini nilikuwa nahudhuria kliniki kwa ajili ya kuangaliwa maendeleo yake,” anasema Kanyenye.

Baba mzazi wa mtoto huyo Bakari Simba anasema mwanzoni alipata wasiwasi juu ya mtoto wake lakini alipopata elimu kuwa tatizo hilo linatibika alihimiza apelekwe kliniki muda ukifika ili anapoendelea kukua asipate changamoto ya kushindwa kutembea.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button