Miundombinu mipya kuongeza masomo ya afya MUHAS

DAR ES SALAAM: CHUO KIKUU cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimesema kinatarajia kuongeza upanuzi wa uwezo wa udahili wa wanafunzi katika fani za afya, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu mipya na ya kisasa kupitia Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi ( HEET).

Mkuu wa MUHAS, Profesa David Mwakyusa amesema kutokana na uhaba wa miundombinu, katika kila wanafunzi 31 wenye sifa za kusoma chuoni hapo, mwanafunzi mmoja tu ndiye anayepata nafasi. Amesema mwaka wa masomo 2025/2026, kati ya waombaji 31,026 waliokuwa na sifa, 986 sawa na 3% ndio walichaguliwa katika kozi mbalimbali za shahada za awali.

Akizungumza jana katika mahafali ya 19 ya chuo hicho, Prof Mwakyumba amesema kupitia mradi wa HEET, ujenzi wa kumbi za mihadhara zenye uwezo mkubwa, maabara, maktaba, mabweni, na miundombinu ya TEHAMA utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya uhaba wa miundombinu kwa kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya mara mbili.

“Matokeo yake, MUHAS itakuwa na uwezo wa kutoa wataalamu wengi zaidi wa afya kwa ubora stahiki, watakaosaidia kuboresha huduma za afya katika hospitali na vituo vya afya nchini kote. Hivyo, mradi huu unachangia moja kwa moja katika kuongeza nguvu kazi ya sekta ya afya nchini Tanzania, sambamba na kutekeleza dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwekeza katika elimu bora, afya bora, na uchumi shindani,” amesema Prof Mwakyusa.

Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS, Harrison Mwakyembe, amewapongeza wahitimu na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na wadau mbalimbali wa elimu, kutoka ndani na nje ya nchi, kwa mchango mkubwa unaoiwezesha MUHAS kutekeleza majukumu yake katika ufundishaji, utafiti na utoaji wa huduma kwa jamii.

Ameeleza pia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika elimu ya juu kupitia Mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi (Higher Education for EconomicTransformation – HEET). Aidha, amesisitiza kuwa tafiti zinazofanyika MUHAS zimeendelea kuchangia mabadiliko ya sera na kuboresha huduma za afya nchini.

Akizungumza katika sherehe hizo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa, Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa jumla ya wahitimu ni 1,362. Kati ya hao, 108 wametunukiwa stashahada na stashahada za juu katika fani mbalimbali za afya na sayansi shirikishi, 680 wamepata shahada ya kwanza, 511 wametunukiwa shahada za uzamili, 54 wamehitimu Master of Science (Superspecialization), huku 9 kutunukiwa shahada ya uzamivu (PhD).

Idadi hii kubwa ya wahitimu kuanzia ngazi ya stashahada hadi uzamivu inaakisi juhudi na mafanikio ya MUHAS katika kuzalisha wataalamu wenye weledi na umahiri, watakaolisaidia taifa kuboresha mifumo ya afya na kuendeleza ustawi wa jamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button