Rais wa Namibia ataja maeneo ya ushirikiano kimkakati

RAIS wa Namibia, Nemtumbo Nandi-Ndaitwah ametaja maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na Tanzania ili kukuza uchumi na kutengeneza fursa za ajira.
Amesema hayo Ikulu Dar es Salaam baada ya kuzungumza na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Nemtumbo alisema ajira zitakazotengenezwa zitasaidia wananchi kuendesha maisha yao na kuondoa umasikini sanjari na kupunguza pengo kati ya masikini na matajiri.
Alitaja uchumi wa buluu ni miongoni mwa sekta ambazo zitatengeneza ajira na kukuza uchumi wa nchi hizo kwa kuwa nchi ya Namibia ina uzoefu wa muda mrefu katika sekta hiyo.
“Hata wakati wa uhuru wetu tuligundua sekta ile ya uvuvi ilikuwa haifanyi kwa sababu kulikuwa na uvuvi ambao haukuwa unadhibitiwa, tulipogundua tulitengeneza sera ambazo zimewezesha sekta ya uvuvi kufanya vizuri,” alisema Rais Nemtumbo.
Alisema sekta hiyo imekuwa mhimili wa uchumi wa nchi hiyo kutokana na mipango na sera walizonazo.
Alisema kilimo na ufugaji wa kisasa utaongeza ajira sambamba na uhakika na usalama wa chakula katika mataifa hayo.
“Kuzielewa mbegu tunazozitumia, udongo pia tunahitaji kuelewa eneo zima la mifugo na viumbe vya baharini hivyo tutaongelea kilimo biashara ambacho ni cha umuhimu sana katika kukuza uchumi wetu,” alisema.
Nemtumbo alisema iwapo madini yataongezwa thamani katika nchi husika kabla ya kusafirishwa kwenda nchi za nje itasaidia kuongeza ajira kwa wananchi.
“Hatuwezi kuendelea kama nchi au bara kuruhusu rasilimali zetu ziende kuongezwa thamani katika nchi nyingine ikimaanisha kuwa kule tunapeleka ajira ambazo zingewafaa vijana wetu,” alisema.
Aliongeza: “Kuongeza thamani na mnyororo wa thamani ni vitu ambavyo inabidi tuvitazame kwa jicho la umakini zaidi kwa kuhakikisha tunaweza kuzalisha bidhaa zenye ubora uleule”.
Alisema kwa kutumia madini ya uraniamu ambayo yanazalishwa kwa wingi nchini Namibia nchi hizo zitakuwa na uwezo na uhakika wa kuzalisha nishati ya kutosha na kuimarisha biashara katika nchi hizo.
Alisema amekubali kutuma Waziri wa Biashara na Viwanda ili aje Tanzania kuona namna nchi hiyo inaweza kushirikiana na kushawishi wafanyabiashara kushiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.