Rais Samia ameahidi, ametekeleza, apewe maua yake

KATIKA hotuba yake bungeni Aprili 22, 2021, pamoja na mambo mengine, Rais Samia Suluhu Hassan aliweka bayana kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itaendeleza na kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

Kwa maneno yake bungeni, Rais Samia alisema, “nami nataka, hapa mwanzoni kabisa, nilieleze Bunge hili tukufu pamoja na Watanzania kwa ujumla, kuwa Dira na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita itakuwa, “Kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya”.

Alilieleza Bunge kuwa kimsingi, hiyo ndiyo dhana na maana halisi ya kaulimbiu/salamu yetu ya ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – Kazi Iendelee’.

Hakuishia hapo alisema serikali yake itaenzi na kuendeleza mambo yote mazuri, lakini pia kufanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kukuza ufanisi na tija.

Na katika hilo, akabainisha kuwa mtangulizi wake Dk John Magufuli aliweka wazi mambo mengi muhimu ambayo yangepewa kipaumbele alipohutubia Bunge Novemba 13, 2020 kwenye miaka hii mitano, mambo mengi ambayo serikali anayoiongoza imepanga kuyatekeleza ni yale yaliyoelezwa na Dk Magufuli akilizindua Bunge.

Rais Samia ametembea katika maneno yake. Jana amefanikiwa kuandika historia nyingine katika Tanzania, katika kutekeleza yale aliyoyaahidi bungeni.

Amezindua Daraja la Kigongo – Busisi, daraja lenye urefu wa kilometa tatu na barabara zake unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 – daraja refu kuliko yote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, na la sita barani Afrika.

Hii ni moja ya ahadi yake katika hotuba yake bungeni. Alieleza kuwa serikali yake itakamilisha pia ujenzi wa madaraja makubwa likiwamo la Kigongo – Busisi, Wami, Tanzanite na Pangani. Jana ametimiza la Kigongo – Busisi ikiwa ni miezi michache baada ya kukamilisha la Tanzanite na Wami na sasa anaelekea kulimaliza la Pangani.

Na amefanya haya baada ya kukamilisha kazi nyingine kubwa ya kuzindua usafiri wa Reli ya Kisasa (SGR) wa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma, na sasa reli hiyo inaendelea kwa kasi kwa vipande vingine vikiwamo alivyoanzisha yeye ujenzi wake.

Wakati jana amezindua Daraja la Kigongo – Busisi, Rais Samia amekamilisha mradi mwingine mkubwa – Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115, ambao sasa unasubiri uzinduzi rasmi.

Haya yote yanadhihirisha wazi kuwa Rais Samia ni mtu wa vitendo. Hakusikiliza maneno ya kukatishwa tamaa, bali alisimama imara kuhakikisha kila kilichoahidiwa na mtangulizi wake kinakamilishwa. Ni Rais wa vitendo.

Kwetu sisi tunaona fahari kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake Rais Samia inatekeleza kwa vitendo mambo mengi iliyoahidi, na imefanikiwa na sehemu nyingine imevuka malengo iliyoahidi.

Kwa msingi huo, kwa kukopa maneno ya sasa ya mtaani, Rais Samia anastahili kupewa maua yake. Ameahidi, ametekeleza na Kazi Iendelee.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button