Sera yataja changamoto elimu awali, msingi

SERA ya Elimu na Mafunzo 2024 Toleo la 2023 imeeleza kuwa mazingira ya elimu ya awali nchini hayaridhishi.

Sera hiyo pia imeeleza kuwa wahitimu wa darasa la saba ni wadogo hivyo hawawezi kujitegemea.

Kwa mujibu wa sera hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Februari Mosi, mwaka huu kuna upungufu wa walimu wa elimu ya awali wenye sifa na miundombinu stahiki.

Advertisement

Imetoa mfano kuwa wastani wa uwiano wa mwalimu na mwanafunzi ulikuwa 1:94 kwa mwaka 2022 badala ya 1:25 unaotakiwa.

Sera hiyo imeeleza kuwa darasa la elimu ya awali kwa sasa lina wastani wa wanafunzi 80 ambao ni zaidi ya mara tatu ya uwiano unaotakiwa.

Imeeleza kuwa muundo wa elimu na mafunzo uliopo unatoa fursa ya mtoto kujiunga na elimu ya awali kwa muda wa miaka miwili lakini uchambuzi unaonesha kuwa mtaala unaotumika unaweza kufundishwa kwa mwaka mmoja kama ukifundishwa kwa ufanisi.

Sera imeeleza kuwa kwa mujibu wa itifaki ya Dakar ya mwaka 2000 ambayo Tanzania imeiridhia ya mwaka 2011 elimu ya awali inatakiwa kutolewa kwa watoto wenye umri kati ya miaka mitatu hadi sita.

Elimu ya msingi Sera imeeleza kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Sura 353, elimu ya msingi ya sasa ni ya miaka saba na ni ya lazima kwa uandikishaji na mahudhurio.

“Hivyo, wahitimu wengi wa elimu ya msingi katika mfumo wa sasa wanakuwa na umri wa miaka 13. Baadhi ya wahitimu huendelea na elimu ya sekondari na mafunzo ya ufundi na wanaokosa fursa hizo huingia kwenye ulimwengu wa kazi,”imeeleza.

Imeongeza: “Wahitimu hawa wanakuwa na umri mdogo na hawana maarifa na ujuzi unaotosheleza kujiunga na ulimwengu wa kazi au kukabiliana na changamoto za maisha pale wanapokosa fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari au elimu ya ufundi.”

Sera imeeleza kuwa mkataba wa kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) umeweka umri wa chini wa kuajiriwa katika baadhi ya kazi kuwa miaka 15.

Imeeleza kuwa kutokana na changamoto za muundo uliopo wa 2+7+4+2+3+ na makubaliano hayo serikali kwa kushirikisha wadau wa elimu imeona umuhimu wa kurekebisha muundo wa elimu ya awali ili itolewe kwa kipindi cha mwaka mmoja, elimu ya msingi kwa miaka sita na elimu ya sekondari chini kwa miaka minne.

Imeeleza kuwa elimu hiyo itakuwa ya lazima na itamwezesha mwanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, kuwa na ufahamu wa jumla na pia kupata umahiri yakiwemo maarifa na ujuzi kulingana na matakwa ya ngazi hiyo.

“Serikali itaendelea kutambua elimu ya awali kuwa sehemu ya mfumo rasmi wa elimu na kuandaa utaratibu wa kuifanya kuwa ya lazima na kutolewa kwa watoto wenye umri wa miaka mitano kwa kipindi cha mwaka mmoja,” imeeleza sera hiyo.

Imeongeza: “Elimu ya awali itajumuisha malezi na makuzi ya mtoto kwa lengo la kumuandaa kimwili, kiakili,
kihisia na kijamii ili kumwezesha kuishi na jamii na kujiunga na elimu ya msingi”.

Serikali itaweka utaratibu wa elimu ya msingi na sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne kuwa ya lazima na itatolewa kwa miaka 10 na pia umri wa kuanza darasa la kwanza utakuwa miaka sita.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *