WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali inatambua kuwa ili kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Geita Gold Refinery (GGR) kifanye kazi kwa ufanisi, kinahitaji upatikanaji wa dhahabu ya kutosha (feed stock) na kwamba Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati ya kufanikisha jambo hilo.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza katika semina iliyoandaliwa kwa ajili ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mavunde amebainisha kuwa Serikali imeshafanya kikao cha pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na wadau wote muhimu ili kuweka mfumo mzuri wa upatikanaji wa mitaji kwa Watanzania kupitia mpango wa Export Credit Guarantee Scheme(ECGS).
Aidha, Waziri Mavunde amesema Serikali inaendelea na juhudi za kuhamasisha wachimbaji wadogo kuanza kuuza dhahabu yao katika viwanda vya ndani ikiwemo GGR, jambo ambalo litawanufaisha kwa kupata bei nzuri, kupunguza gharama za usafirishaji, na kufurahia punguzo la tozo zilizowekwa kwa dhahabu inayosafishwa ndani ya nchi.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa hapa nchini yanaongezewa thamani hapahapa nchini, hatua inayolenga kuongeza mapato ya Serikali, kutoa ajira kwa Watanzania, na kusaidia sekta nyingine zinazohusiana na madini, kama vile benki na viwanda vya vifaa vya uchimbaji kuendelea kupata masoko.
Amesisitiza kuwa, GGR ni kiwanda cha kisasa chenye hadhi ya kimataifa ambacho kimekuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini nchini.

“Tuna furaha kuona kwamba sasa Tanzania inayo miundombinu ya hali ya juu kwa ajili ya usafishaji wa dhahabu, jambo ambalo linaipa nchi yetu hadhi kubwa katika soko la madini duniani,” amesema Mavunde.
Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge kuwa, Serikali inajivunia uwepo wa viwanda vya uongezaji thamani.