Sh Bilioni 3.4 kujenga kiwanda cha parachichi

IRINGA; Ndoto ya kujenga kiwanda cha parachichi katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa, imeanza kutimia baada ya serikali kutangaza kukamilika kwa taratibu za ujenzi wake utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 3.4.

Kiwanda hicho, ambacho ni mradi wa serikali kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kutatua changamoto ya soko, kubadilisha maisha ya wakulima na kuchangia pato la Taifa.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/bashe-aagiza-kukamatwa-mnunuzi-wa-parachichi/

Advertisement

Akitoa taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na wananchi wa wWlaya ya Mufindi, Naibu Waziri Kilimo, David Silinde amesema wiki ijayo mkandarasi atafika eneo la mradi tayari kwa maandalizi ya ujenzi wake.

“Ili kuwawezesha wakulima wengi kuingia katika kilimo cha zao hili, serikali imeweka ruzuku katika picha ya parachichi hatua itakayowezesha kuuzwa kwa Sh 2500 tu badala ya Sh 20,000,” amesema Silinde.

Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika mikutano yake miwili tofauti aliyofanya katika Kijiji cha Ilamba na Wambi mjini Mafinga, alisema baada ya kugundua kuwa parachichi ina mahitaji makubwa hasa katika nchi za Ulaya na Asia, serikali iliamua kuwekeza katika mradi huu.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/ziara-ya-chongolo-mufindi-kiwanda-cha-parachichi-kujengwa/

Amezitaka mamlaka na wadau wa kilimo hicho kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima juu ya mbinu bora za kilimo cha parachichi, ikiwemo upandaji, utunzaji wa mimea, na uvunaji.

Mbali na kiwanda hicho kuongeza soko la zao hilo nchini, Majaliwa amesema lina soko la uhakika katika nchi za China na India na akawataka wananchi walioko katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Ruvuma ambako kuna ardhi nzuri kwa kilimo hicho kuichangamkia fursa hiyo.

“Wananchi ingieni katika kilimo hiki na niwahakilishie hakuna parachichi itakayotupwa hata kama itaoza. Zote zitapata soko kulingana na mahitaji yake,” amesema.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/serikali-yahimiza-kilimo-cha-maparachichi/

Akizungumzia ukubwa wa kiwanda hicho, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema kinatarajiwa kuwa na sehemu kuu tatu ikiwemo ya usindikaji itakayohusika na upokeaji, usafishwaji na upangaji wa madaraja.

Sehemu nyingine ni ya ufungashaji kwa viwango vya kimataifa tayari kwa kusafirishwa na kitengo cha utafiti na maendeleo kitakachokuwa na jukumu la kuendeleza teknolojia mpya na kuboresha mbinu za uzalishaji.

Isome pia:https://habarileo.co.tz/kenya-yapata-soko-la-parachichi-china/

Akizungumzia neema kwa wananchi, Kigahe alisema kiwanda hicho kitaleta manufaa makubwa kwa wakazi wa mkoa wa Iringa na mikoa yote inayolima zao hilo kwa kuongeza ajira, kipato, maendeleo ya miundombinu mbalimbali kama barabara, na huduma za maji, na kuchochea biashara ndogondogo.