Tanzania, Nambia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi

TANZANIA na Namibia zimekubaliana kuongeza nguvu katika ushirikiano wa kiuchumi.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema ingawa ushirikiano katika maeneo mengine umeimarika bado ushirikiano wa uchumi na biashara upo chini na kuna fursa ya kuukuza.
Amesema hayo Ikulu Dar es Salaam alipozungumza na wanahabari baada ya kumkaribisha nchini Rais wa Namibia, Dk Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Rais Samia alisema licha ya kiwango cha biashara kati ya Namibia na Tanzania kupanda kutoka Sh bilioni 17 hadi bilioni 20 kati ya mwaka 2019 hadi 2023 bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi.
“Tunafahamu kwamba kuna wafanyabiashara wachache ambao wanafanya biashara Namibia, lakini vilevile kuna wafanyabiashara wachache na wawekezaji wachache ambao wamewekeza ndani ya Tanzania, tumekubaliana kuangazia eneo hilo,” alisema.
Rais Samia amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Namibia waje kushiriki katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba, mwaka huu ili waje kuzungumza na wenzao na waone namna ya kuanza ushirikiano na kuyabainisha maeneo ya ushirikiano.
Ameagiza mamlaka husika za uwekezaji ziendelee kuratibu makongamano ya biashara kati ya Tanzania na Namibia ili kurahisisha matumizi ya fursa za kikanda katika kuhamasisha soko huru la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Aidha, Rais Samia alitaja maeneo ya ushirikiano waliyokubaliana kuwa ni uongezaji wa thamani wa mazao ya mifugo, uvuvi na pia katika sekta ya utalii.
“Kubwa tumeomba kujifunza kutoka kwao hasa kwenye sekta ya mifugo kwa sababu Namibia ni wauzaji wazuri wa ulimwenguni hivyo tumeomba kujifunza kutoka kwao,” alisema.
Rais Samia alisema katika eneo la gesi na mafuta wamekubaliana kushirikiana maeneo yote kwa sababu nchi zote mbili zina gesi nyingi huku Namibia wakianza kuona mafuta.
Pia, alisema eneo lingine ni uchumi wa buluu kwa sababu ni sekta inayokuza uchumi na kuwezesha kukabiliana
na ukosefu wa ajira. Namibia ni mfano bora Afrika yenye utawala mzuri wa rasilimali za bahari.
Kwa upande wa ushirikiano kwenye utamaduni, walikubaliana kushirikiana katika Lugha ya Kiswahili kama kilivyotumika katika mapambano ya kudai Uhuru basi iendelee kutumika kuwaunganisha watu wa nchi zote mbili.
Alisema jambo muhimu ni hatua ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kushirikiana na chuo kingine cha Namibia wamekubaliana kuanza kufundisha Kiswahili ngazi ya chuo.
Alisema wamekubaliana pia kukuza uhusiano kupitia jumuiya za kikanda kama SADC na Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN).