TSN, Xinhua kuimarisha ushirikiano matumizi AI

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) na Shirika la Habari la China, Xinhua News Agency zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kihabari kwa njia ya kubadilishana maudhui, kutumia teknolojia ya Akili Mnemba (AI) hasa katika tasnia ya habari.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za TSN jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TSN, Asha Dachi, amesema uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na umeanza kabla ya uhuru wa Tanganyika, na kusisitiza kuwa TSN iko tayari kushirikiana na China, hususan katika matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo AI, bila kuathiri maadili na sera za uhariri wa ndani.
“Tunaukubali ujio wa teknolojia kama AI, lakini tunahitaji mafunzo zaidi kwa wafanyakazi wetu ili kuhakikisha matumizi yake yanaendana na sera zetu za habari,” alisema Dachi na kupendekeza kuimarishwa kwa vifaa na msaada wa kitaalamu hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Xinhua nchini Tanzania, Hua Hongli, ameeleza kuwa shirika lao tayari linatumia AI katika kazi za kihabari kupitia ofisi yake iliyoko Nairobi, Kenya, na kuahidi kuwa wako tayari kushirikiana na TSN kwa kutoa mafunzo ya matumizi ya AI kwa waandishi wa habari nchini.
“Tuna mifumo ya AI inayotumika na waandishi wetu. Tunaweza kuleta wataalamu Tanzania kupitia ofisi yetu ya Nairobi ili kutoa mafunzo,” amesema Hongli.
Amesema ushirikisno huo unaweza kujumuisha maudhui ya picha, habari na video kwa lugha mbalimbali, na kwamba kuna historia ya makubaliano ya kuchapisha maudhui ya Xinhua kupitia gazeti la Daily News, ambayo yanaweza kufufuliwa.
Katika kikao hicho, Kaimu Meneja wa Huduma za Habari kwa Lugha za Kigeni, Christopher Majaliwa, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha taarifa sahihi ndizo zinazoingizwa kwenye mifumo ya AI.
“Tunahitaji kuweka taarifa zetu katika injini ya AI ili kudumisha uaminifu,” amesema.
Naye Kaimu Meneja wa Huduma za Vyombo vya Habari kwa Njia ya Kidijitali, Sylvester Domasa, amehimiza kuwepo kwa juhudi za pamoja katika kuboresha utofauti wa maudhui, ambapo amesema “Kwa kushirikiana na kubadilishana uzoefu, tunaweza kuunda mazingira jumuishi na bora zaidi ya vyombo vya habari kati ya mataifa yetu,”