Tuendelee kuongeza nguvu sekta ya utalii

MOJA ya malengo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 ni kuimarisha sekta mbalimbali za kiuchumi ili kuliwezesha taifa kupata fedha za kuwaletea wananchi maendeleo.

Moja ya sekta hizo ni utalii, ambayo CCM katika ilani yake hiyo ya uchaguzi imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi itaweka mkazo katika kupanua wigo wa bidhaa/mazao ya utalii ili sekta hiyo iendelee kuchangia zaidi katika Pato la Taifa.

Katika kutekeleza lengo hilo, Ilani imefafanua kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itatekeleza mambo kadhaa ikiwamo kubuni na kutekeleza mikakati ya kuongeza na kukuza wigo wa bidhaa/mazao ya utalii ili kufikia watalii milioni tano kwa mwaka kufikia mwaka 2025 na kuongeza mapato kutoka Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani bilioni 6.0 mwaka 2025.

Advertisement

Tayari mambo kadhaa yamefanyika katika kuelekea kufikia malengo hayo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ikiwamo Rais Samia Suluhu Hassan kushiriki na kuzindua filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ ambayo ilizinduliwa nchini Marekani na maeneo kadhaa nchini. Matunda ya filamu hiyo yameonekana na ni makubwa sana.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa juzi na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), filamu hiyo imehamasisha na kuongeza watalii kuingia nchini kutoka 456,266 hadi kufikia 742,133 sawa na ongezeko la asilimia 62.7. Ongezeko la idadi ya watalii limetokea katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2021.

Wakati filamu hiyo ikiongeza watalii nchini, pia juzi sekta ya utalii ilipata nguvu nyingine baada ya serikali kukabidhi malori 44 kwa Shrika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) chini ya Mradi wa Kuendeleza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Mradi huu utakuwa na manufaa kwa wananchi zaidi ya 40,000 wa vijiji 61 vinavyozunguka hifadhi za taifa za Udzungwa, Nyerere, Ruaha na Mikumi kupata ajira na kukuza pato lao la kiuchumi. Lakini pia kuendeleza utalii katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

Hizi zote ni juhudi za kuendeleza utalii kama ilivyoelekezwa chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwa hakika juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda na hakuna shaka zikiendelea, malengo yaliyoainishwa katika ilani hiyo yatafikiwa na kuvukwa itakapofika au kabla ya 2025.

Ndio maana tunaungana na serikali kuwahimiza Watanzania kuendeleza juhudi za kuimarisha utalii nchini ili kuiwezesha nchi kupata fedha zitakazokwenda kuwahudumia hasa katika masuala ya huduma za kijamii na sekta nyingine zikiwamo za usafiri.

Hakuna ubishi kuwa sekta ya utalii ikisimamiwa vizuri itaendelea kukua na kutoa mchango zaidi katika Pato la Taifa, hivyo juhudi zinazofanywa na Rais Samia na serikali yake, zinapaswa kuungwa mkono na Watanzania wote wanaoitakia mema nchi yao. Watanzania waendelee kuwa wakarimu kwa wageni wanaotembelea vivutio mbalimbali nchini na pia wawe mabalozi wema wa kuvitangaza, kuvitunza na kuviendeleza vivutio hivy