Wahitimu Dk Salim Ahmed Salim washauriwa kujiajiri

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amewataka wahitimu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim kutengeneza mazingira ya kijiajiri kulingana na ujuzi walioupata.

Akizungumza leo kwa niaba ya Waziri wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Januari Makamba, katika mahafari ya 26 ya kituo hicho, Balozi Mbarouk Nassor ameweka wazi ugumu wa soko la ajira hivyo kwa kufanya hivyo wahitimu hao watatengeneza mazingira ya kuajiri na wengine.

“Wakati mnaendelea na harakati za kutafuta ajira napenda kuwashauri kutumia ujuzi wenu kujiajiri, jiwekeeni malengo makubwa yatakayowapa uwezo wa kuawaajiri Watanzania wengine waliopo maeneo mbalimbali.” Amesema Balozi Mbarouk.

Aidha kwa kutambua changamoto za mitaji kwa vijana, Balozi Mbarouk amesema serikali imeelekeza kila halmashauri kutengea mikopo kwa vikundi vya vijana wajasiriamali.

Balozi Mbarouk amekishauri kituo hicho kuboresha programu zake ili kukidhi mahitaji ya wizara na taifa, pia kutoa elimu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na uhusiano wa kimataifa na diplomasia ya uchumi.

Mara baada ya hotuba yake, Balozi Mbarouk aliwatunuku wanafunzi 1008 waliohitimu ngazi mbalimbali, ya Astahahada Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Stashahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Stashahada ya juu Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia.

Wahitimu wengine ni ngazi ya Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia, Stashahada ya Uzamili ya Menejiment Uhusiano wa Kimataifa, Stashahada ya Uzamili Diplomasia ya Uchumi, Stashahada ya Uzamili ya Amani na Menejimenti ya Migogoro, na Shahada ya Uzamili Utawala wa Kimkakati.

Ramadhan Ismail mhitimu wa Shahada ya Uzamili Utawala wa Kimkakati amesema atatumia ujuzi aliopata kufanya kazi kwa weledi ili taifa linufaike na elimu yake, sambamba na hilo amewashauri wahitimu wenzake kushirikiana ili kuleta matokeo mazuri kwa taifa.

“Kwa kiasi kikubwa nchi inatugemea kwa hiyo tufanye kazi kwa bidii, tushindane ila katika mambo chanya maana nchi yetu haiwezi kwenda mbele bila sisi.”Amesema Ramadhan Ismail.

Septemba 30, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alibadili jina Chuo cha Diplomasia na kuitwa Dk Salim Ahmed Salim.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button