Wajengewa uwezo utambuzi viumbehai vinavyotoweka

UMOJA wa Nchi za Ulaya (EU) kupitia Mradi wa Erasmus+CONTAN umefanikiwa kuwajengea uwezo wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu vitatu na kuwa na uwezo mkubwa wa kiubobezi kufanya tafiti za kutambua viumbe hai vilivyokaribuni kutoweka nchini.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), upande wa Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Amandus Muhairwa amesema hayo akiwa mjini Morogoro wakati wa kongamano la wadau wa vyuo vikuu vya nje ya nchi na vya ndani ambavyo ni SUA, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM).

Profesa Muhairwa amesema licha ya wataalamu wakiwemo walimu na wale wanaohusika na bioanuwai kujengewa uwezo zaidi katika kupima na kuhifadhi sampuli za viumbe hai , pia mradi umeleta vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufundishia na kufanyia utafiti.

“Mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye chuo chetu ni kuwezesha walimu kufundishwa katika bioanuwai katika kiwango cha kimataifa zaidi na pia kupata vifaa vya kufundishia ikiwemo hadubini za kufanyia utafiti “ amesema,” Profesa Muhairwa.

Naye mmoja wa waratibu wa mradi huo ,Dk Charles Kilawe ambaye ni Mhadhiri wa SUA amesema mradi huo umefadhiliwa kwa asilimia 100 na EU na kufanyika katika Chuo Kikuu hicho na vingine viwili kwa kipindi cha miaka minne kuanzia 2021 hadi 2024.

SOMA: SUA kuakisi maendeleo

Dk Kilawe amesema mradi huo haukuwa wa kiutafiti ,bali ni wa kujenga uwezeshaji kwa walimu na wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya tafiti za kisasa kwenye maeneo ya bioanuwai kupima na kuhifadhi.

Mratibu wa mradi huo alisema kupitia mradi huo vifaa mbalimbali vimenunuliwa zikiwemo harubini za kisasa , majenereta , makabati ya kuhufadhia sampuli kavu za mimea na wadudu.

“ Sampuli hizi kavu zinatumia kwenye utafiti na kufundishia wanafunzi wetu namna ya kutambua zile bioanuwai zipo hatarini na namna ya kuzilinda kwa kushirikiana na wahifadhi wa wanyamapori na wahifadhi wa misitu“ amesema Dk Kilawe.

SOMA: SUA yaeleza mafanikio miaka mitatu ya Samia

Pia amesema mradi umewawezesha wahifadhi wa Wanyamapori pamoja na hifadhi za misitu ambao wamepewa elimu hiyo namna ya kutambua hatari zilizipo kwa viumbe adimu na namna ya kuhifadhi.

Kwa upande wake Mkufunzi Msaidizi wa Idara ya Utunzaji na usimamizi wa mifumo ya Ikolojia kutoka SUA , Hadija Mchelu alisema mradi huo umewazesha wanafunzi uwezo mkubwa utakaowasaidia kufanya tafiti na kubaini viumbe hai na kuzihifadhi.

“ Nikiwa mmoja wa Mwanafunzi niliyenufaika na mradi huu niliweza kusoma kozi mbalimbali ikiwemo kujifunza namna ya kukusanya taarifa za viumbe hai (biodiversity monitoring data collections) ambazo zitatusaidia katika kufanya tafiti na kuandaa machapisho ya kisayansi,” amesema Hadija.

Habari Zifananazo

Back to top button