‘Twenzetu Kileleni’ kuadhimisha Uhuru Tanganyika
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limezindua msimu wa nne wa kampeni ya Twenzetu Kileleni huku wakihimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupanda Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara Tanapa Jully Lyimo amesema kampeni hiyo ni sehemu ya kuadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika katika sura ya utalii itayofanyika Desemba 9.
“Tunafahamu kuwa kila ifikapo Desemba 9 nchi yetu huadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika, kama Tanapa tumekuwa tukitumia siku hii kutangaza utalii wa hifadhi ya taifa ya Mlima wa Kilimanjaro, watanzania waende kupanda,”alisema.
Alisema upandaji huo ulianza tangu mwaka 1961 wakati nchi ikipata uhuru ambapo ambapo Kapteni wa Jeshi la Wananchi wakati huo Alexander Nyirenda alipandisha mwenge kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Lyimo amesema zoezi hilo liliendelea likiongozwa na viongozi wakuu wa Jeshi la Wananchi akiwemo Jenerali mstaafu Mrisho Sarakikya na baadaye Jenerali Mstaafu George Waitara.
SOMA: TANAPA yajivunia miaka mitatu ya Rais Samia
Amesema kuanzia mwaka 2021 kupitia upandaji huo walianzisha kampeni hiyo ikwa imelenga kuhamasisha Watanzania kupanda mlima ikiwa ni ishara ya uzalendo na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii.
“Kwa kuwa mwaka huu ni msimu wa nne wa kampeni hiyo, tunatoa hamasa kwa watu binafsi, watanzania ndani na nje ya nchi, mabalozi, taasisi za Serikali na binafsi kujitoa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizi,”amesema.
Kwa upande wake Ofisa Uhifadhi Mkuu wa Tanapa Mapinduzi Mdesa alisema katika upandaji huo kuna maeneo mengi ambayo ni kivutio kama maporomoko ya maji na kuwaita Watanzania kutumia fursa hiyo kutembelea.
SOMA: Watumishi Tanapa kupewa mafunzo ya kijeshi
Amesema kuna shughuli mbalimbali ambazo hufanyika kama upandaji wa parachute, utalii wa michezo, mpira wa miguu umekuwa ukifanyika, mbio za baiskeli na kuvunja rekodi mbalimbal ikiwemo kupanda bila viatu, kutembea na jokofu mgongoni.
“Katika maadhimisho haya tutatumia njia tatu Marangu, Machame na Lemosho kupanda kwenye mlima,”amesema na kutaja kauli ya mbiu ya mwaka huu stawisha uoto wa asili Tanzania okoa barafu ya Mlima Kilimanjaro.
Muongoza wageni Kampuni ya utalii ya ZARA Faustin Chombo ameishukuru serikali kwa kuwaunga mkono akisema mwaka jana walipata wageni 200.
SOMA: Hakuna nyaraka sahihi malipo Sh Bil 1.95 Tanapa
Amesema gharama za upandaji kwenye mlima huo ni Sh milioni 1.5 kwa kila mpandaji huku wakizibeba gharama za chakula, malazi kwa siku tatu ambapo mwaka huu wamepanda kusimika bendera ya Taifa kileleni Desemba 5, mwaka huu.